IQNA

Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani

Qari wa Niger asema Qur'ani Tukufu imeleta maana katika maisha yake-Video

14:13 - February 21, 2024
Habari ID: 3478387
IQNA – Hafidh wa Qur'ani Tukufu kutoka Niger ambaye ameshiriki fainali ya Awamu ya 40 ya Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran alisema kujifunza Qur'ani kumebadilisha maisha yake.

Obaidullah Abubakr Ango ameyasema hayo katika  mahojiano na Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA) kando ya mashidano hayo jijini Tehran na kuongeza kuwa, kujifunza Qur'ani Tukufu na kuitafakari kumebadilisha maisha yake na kuyapa maana mpya.

Alisema aliona kuwa ni baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kujifunza na kuhifadhi Qur'ani Tukufu.

Alimsihi yeyote anayetafuta njia ya kubadilisha maisha yake kuwa bora kurejelea kitabu hiki cha Kitukufu.

Obaidullah alisisitiza haja ya kujumuisha mafundisho ya kimaadili na akhlaqi ya Qur'ani Tukufu katika mfumo wa elimu, na kuongeza kuwa kizazi kilicholelewa na maadili ya Qur'ani kinaweza kuandaa njia ya mabadiliko ya kweli katika Umma wa Kiislamu.

Alipoulizwa kuhusu shughuli za Qur'ani nchini Niger, alisema kuna mapokezi mazuri miongoni mwa watu wa rika tofauti kwa ajili ya kozi za Qur'ani zinazotolewa katika vituo vya kuhifadhi Qur'ani nchini humo.

Alisema baadhi ya vituo hivyo vinatumia mbinu mpya za kufundishia Quran huku vingine vikitumia njia za jadi.

Obaidullah alibainisha kwamba alianza kujifunza kuhifadhi Qur'ani akiwa na umri mdogo kwa msaada wa baba yake.

Baada ya kuhifadhi Qur'ani nzima, aliendelea kujifunza Tajweed na sheria za usomaji hadi umri wa miaka 15 na kwa sasa ni mwalimu wa Qur'ani.

Alibainisha kuwa mafunzo ya Qur'ani nchini Niger yameathiriwa kwa kiasi kikubwa na nchi jirani ya Nigeria.

Hii hapa chini ni qiraa ya Obaidullah Abubakr Ango katika Mashindano ya Qur'ani

Hadi sasa ameshiriki katika mashindano manne ya kimataifa ya Qur'ani nchini Tanzania, Kenya, Senegal na Misri na kumaliza wa kwanza katika mashindano ya Tanzania.

Alipoulizwa kuhusu mashindano ya Qur'ani ya Iran, amebaini kuwa kiwango mashindano ni kizuri sana.

Pia alisifu ubora mzuri wa mpangilio wa hafla hiyo na umahiri wa wajumbe wa jopo la majaji.

Fainali ya Awamu ya 40 ya Mashindano ya kimataifa ya Qur'ani ya Iran  ilizinduliwa mjini Tehran siku ya  17 Februari na inamalizika leo Februari 21.

Jumla ya wahifadhi na wasomaji 69 kutoka nchi 44 wanashindana katika fainali katika kategoria kuu za usomaji wa Qur'ani (kwa wanaume) na kuhifadhi Qur'ani na usomaji wa Tarteel (kwa wanaume na wanawake).

Hafla hiyo ya kila mwaka, inayoandaliwa na Jumuiya ya Masuala ya Wakfu na Misaada, inalenga kukuza utamaduni na maadili ya Qur'ani miongoni mwa Waislamu na kuonyesha vipaji vya wasomaji na wahifadhi Qur'ani.

/3487270

Habari zinazohusiana
captcha