IQNA

Wiki ya Umoja wa Kiislamu

Ukuruba wa Iran-Saudia 'Mfano wa Kuigwa' katika ushirikiano wa kikanda

20:13 - October 01, 2023
Habari ID: 3477678
TEHRAN (IQNA) - Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu amekaribisha kuanzishwa tena kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia kama maendeleo muhimu ya ushirikiano na urafiki kati ya nchi zote za Kiislamu.

Hujat-ul-Islam Hamid Shahriari aliyasema hayo katika hotuba yake ya ufunguzi wa Kongamano la 37 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu lililofanyika leo Jumapili mjini Tehran.

Alisifu hatua hiyo ya nchi mbili kama "mfano wa kuigwa" kwa nchi nyingine za kanda na ishara ya kuelewa kwamba madola ya nje ya ulimwengu wa Kiislamu hayataki malengo endelevu katika eneo. Alisema, "Hatua hii inaahidi amani ya muda mrefu na ushirikiano kwa kanda nzima."

Shahriari alielezea matumaini yake kuwa kuboreshwa kwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili kutapelekea ushirikiano katika sayansi na teknolojia, usalama wa kikanda, nguvu za kisiasa na mabadilishano ya kiuchumi na kiutamaduni yenye manufaa. Vile vile ametoa wito wa kukatwa mikono ya maadui kutoka eneo hili kama hitajio la kupatikana kwa Ummah wa Kiislamu ulioungana.

Shahriari amesisitiza umuhimu wa Qur'ani Tukufu kuwa ni mwongozo wa kipekee kwa binadamu unaoleta ujumbe wa urafiki na Waislamu na upinzani dhidi ya madhalimu. Vile vile amesisitiza kuwa ushirikiano baina ya nchi za Kiislamu utahakikisha kupanuliwa uhusiano wa kiuchumi na kidiplomasia na kufungua njia mpya ya mabadilishano ya kiuchumi na kiutamaduni.

Shahriari ameligusia suala la Palestina kuwa ni suala muhimu kwa ulimwengu wa Kiislamu na kusisitiza kuwa, uungaji mkono kwa taifa la Palestina na al-Aqsa tukufu unapaswa kwenda zaidi ya maneno.

Wageni wa mkutano huo ni wanazuoni, wasomi na wanaharakati 110 kutoka nchi 41 na pia wasomi wa hapa nchini Iran.

Mwaka huu, zaidi ya makala 200 kutoka nchi 20 kama vile Misri, Algeria, Tunisia na Iraqi katika lugha tofauti zimetumwa kwa sekretarieti ya mkutano.

Inafaa kuashiria hapa kuwa, Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu Iran hufanyika katika siku tukufu za kuadhimisha Maulid ya Mtume Mtukufu wa Uislamu Mohammad al Mustafa SAW, siku ambazo ni maarufu kama siku za Maulidi. Waislamu wa madhehebu ya Sunni wanaadhimisha siku hiyo tarehe 12 Rabiul Awwal na Waislamu wa Madhehebu ya Shia wanamini siku hiyo ni tarehe 17 Rabiul Awwal.

Miaka mingi iliyopita, Hayati Imam Khomeini MA, Kiongozi mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, ambaye binafsi alikuwa mstari wa mbele kulingania umoja wa Kiislamu alipendekeza kuwa, muda uliopo baina ya tarehe hizo mbili uwe ni "Wiki ya Umoja wa Waislamu" kwa lengo la kuimarisha mashikamano na udugu baina ya madhehebu za Kiislamu.

4172173

Habari zinazohusiana
captcha