IQNA

Iran na Ustawi

Kiongozi wa Mapinduzi: Miaka 40 ya ustawi ni ishara ya usahihi wa uchambuzi wa Mapinduzi

11:02 - October 20, 2022
Habari ID: 3475956
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, maendeleo ya miaka 40 ya nchi yanadhihirisha usahihi wa uchambuzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu dunia mkabala wa uchambuzi wa watu wenye fikra na mielekeo ya Kimagharibi.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo Jumatano mjini Tehran katika kikao cha mamia ya vijana wasomi na wenye vipawa vya juu vya kisayansi nchini Iran waliokwenda kuonana naye. 

Katika kikao hicho, Ayatullah Khamenei ameashiria propaganda zinazoendelea kufanywa na Wamagharibi tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hadi sasa wakidai kwamba Jamhuri ya Kiislamu inaelekea kusambaratika, na kusema: Waliainisha muda wa madai hayo na kila mara walisema mwezi ujao, mwaka mmoja ujao au miaka mitano ijayo Jamhuri ya Kiislamu itakuwa imekwisha; na baadhi ya watu ndani ya nchi walikuwa wakieneza madai haya kutokana na kughafilika au kwa nia mbaya.

Amesisitiza kuwa: "Hatukukata tamaa na tulisimama imara, na Mungu akipenda tutaendelea kusimama kidete."

Akiashiria kuwepo mifumo miwili ya kiuchambuzi katika uwanja huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Mfumo mmoja wa kiuchambuzi unaamini kuwa, kufanya kazi na kusimama kidete dhidi ya kanuni za kiulimwengu na madola yanayotokana na kanuni hizo kama vile Marekani ni jambo lisilo na faida na la kuangamiza; watu hao pia huwaona wale wanaotoa uchambuzi tofauti kuhusu hali halisi ya ulimwengu kuwa wamechanganyikiwa.

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Uchanganuzi wa pili na wa kiuhalisia, huona majmui ya uhalisia wa mambo yote mazuri na mabaya, na kufanya harakati kwa msingi huo.

Amesisitiza kuwa: Jambo la kuzingatiwa ni kwamba, Jamhuri ya Kiislamu imeendeleza harakati inayokwenda kwa kasi kuanzia mwisho wa msafara na hii leo imefika karibu na mbele ya msafara huo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: "Wasomi wetu hawakuruhusu nchi iendelee kuwa tegemezi kwa Wamagharibi." Aidha amesema: "Lengo la madola ya kibeberu duniani ni kueneza satwa yao, wakati moja wanatumia silaha, siku nyingine wanatumia hadaa na pia wakati mwingine wanatumia elimu kueneza satwa yao. Hivyo vyuo vkuu vinapaswa kuzuia satwa hii ya mabeberu. Iwapo vyuo vikuu vitainua viwango cya elimu basi vitaweza kuzuia kujipenyza mabeberu nchini."

Akielezea baadhi ya mafanikio ya wasomi na wanasayansi wa Iran, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduuzi ya Kiislamu ameashiria utafiti na mafanikio ya Taasisi ya Utafiti ya Royan katika nyanja kama vile seli shina na uundaji wa wanyama hai (cloning), maendeleo katika biokemia, kurusha na kuongoza satalaiti katika anga za juu, mafanikio makubwa katika tasnia ya nyuklia, utengenezaji wa chanjo tata zikiwemo chanjo za corona na maendeleo ya kustaajabisha katika uundaji wa makombora na ndege zisizo na rubani (drone).

4092894

captcha