IQNA

Raisi aapishwa na kuwa Rais wa nane wa Iran, asisitiza haki ya kumiliki teknolojia ya nyuklia

21:30 - August 05, 2021
Habari ID: 3474160
TEHRAN (IQNA)- Sayyid Ibrahim Raisi amekula kiapo jioni ya leo na kuwa rais wa 8 wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuahidi kwamba atalinda na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na Katiba ya nchi kwa nguvu zake zote.

Rais Raisi amekula kiapo hicho kwa kitabu kitakatifu cha Qur'ani katika sherehe iliyofanyika katika ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu na kuhudhuriwa na Mkuu wa Idara ya Mahakama, Gholamhossein Mohseni-Ejei, wawakilishi wa Bunge, wanachama wa Baraza la Kulinda Katiba na wageni waalikwa kutoka zaidi ya nchi 70 duniani.

Akizungumza kwa mara ya kwanza akiwa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baada ya kuapishwa Rais Ibrahim Raeisi amesisitiza kuwa, serikali yake itatoa kipaumbele masuala ya matatizo ya kiuchumi ya wananchi, kupambana na ufisadi, kuimarisha sarafu ya nchi na kuendeleza sera za ujirani mwema.

Amesisitiza kuwa, uwepo wa vikosi vya kigeni katika eneo la Asia Magharibi katu hakuwezi kuyapatia ufumbuzi matatizo ya eneo hili. Kuhusiana na kadhia ya miradi ya nyuklia ya Iran, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, taifa hili lina haki ya kunufaika na teknolojia hii na kwamba, kwa mujibu wa itikadi na mafundisho ya Uislamu Tehran inaamini kuwa, ni haramu kumiliki silaha za nyuklia.

Kuhusiana na baraza lake la mawaziri, Rais wa Iran amesema kuwa, kama alivyotilia mkazo Kiongozi Muadhamu kuhusiana na kuharakishwa mwenendo huu, atahakikisha analikabidhi Bunge orodha yake ya mawaziri Bungeni mwanzoni mwa wiki ijayo na kabla ya kumalizika muda wa wiki mbili alionao kwa mujibu wa katiba.

3988675/

 

Kishikizo: iran raeisi
captcha