IQNA

Jinai za Israel

Israel yawaua kinyama makamanda wa Jihad Islami, Wapalestina waapa kulipiza kisasi

17:46 - May 09, 2023
Habari ID: 3476981
TEHRAN (IQNA)- Wapigania ukombozi wa Palestina wameapa kulipiza kisasi baada ya jeshi la utawala haramu wa Israel kuwaua makamanda wa ngazi za juu wa Harakati ya Jihad Islami katika Ukanda wa Gaza.

Alfajiri ya leo, ndege za kivita za Israel zimeshambulia maeneo tofauti ya Ukanda wa Gaza katika hujuma ya kushtukiza.

Wapalestina 13 wameuawa shahidi katika mashambulizi hayo yaliyotekelezwa na makumi ya ndege za kivita za Israel, 9 kati yao wakiwa ni wanawake na watoto.

Wizara ya Afya ya Serikali ya Ukanda wa Gaza imetangaza kuwa Wapalestina 13 wameuawa shahidi na zaidi ya watu wengine 20, wakiwemo wanawake na watoto kadhaa, wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo. Wanachama watatu wa ngazi za juu wa harakati ya Jihad Islami pia walikuwa miongoni mwa mashahidi.

Msemaji wa jeshi la Israel amesema, ndege 40 za kivita zimeshiriki katika mauaji hayo.

Harakati ya Jihad Islami ya Palestina imetoa taarifa ikitangaza kuwa, adui Mzayuni ndiye anayehusika kikamilifu na mauaji hayo ya kihaini ya kigaidi na kueleza kuwa, adui hatafikia malengo yake kwa jinai hiyo.

Jihad Islami imesisitiza kuwa Saraya Al-Quds, tawi la kijeshi la harakati hiyo, pamoja na mirengo mingine ya muqawama, kamwe haitazembea hata kidogo katika kulipiza kisasi cha damu safi ya mashahidi hao.

Tariq Salmi, msemaji wa harakati ya Jihad Islami pia amesema kuwa, adui Mzayuni atalipa gharama za jinai hiyo na kwamba wapiganaji wa harakati hiyo watatekeleza wajibu wao kukabiliana na jinai hiyo.

Harakati ya Jihad Islami imetangaza kuwa "Jihad Shakir al-Ghannam", katibu wa Baraza la Kijeshi la Saraya Al-Quds, " Khalil al-Bahitini", mjumbe wa Baraza la Kijeshi na Kamanda wa Kaskazini wa Saraya Al-Quds, na "Tareq Mohammad Izzuddin", mmoja wa viongozi wa operesheni za kijeshi za Saraya Al-Quds katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Kwa upande wake, mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestiina (Hamas), Ismail Haniyeh, amesema kuwa "adui amefanya makosa katika tathmini yake na atalipa gharama ya jinai yake," akisisitiza kuwa "muqawama pekee ndio utakaoamua njia ambayo itamuumiza adui."

Haniyeh ameongeza kuwa mauaji ya viongozi wa muqawama kwa operesheni ya kigaidi hayatampa usalama adui mvamizi, na badala yake yatazidisha mapambano. Amesema kuwa "uhalifu huo unawalenga watu wote wa Palestina, na kambi ya muqawama itaungana pamoja katika kukabiliana uhalifu huo."

/3483489

Kishikizo: jihad islami palestina
captcha