IQNA

Mgogoro Sudan

OIC kuandaa mkutano wa dharura Jeddah kujadili mgogoro Sudan

18:50 - May 02, 2023
Habari ID: 3476948
TEHRAN (IQNA) – Mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) umepangwa kufanyika wiki hii kujadili mgogoro unaotokoota nchini Sudan

Mkutano  huo utafanyika kwa ombi la Saudi Arabia, rais wa sasa wa mkutano wa OIC, siku ya Jumatano.

Makao makuu ya OIC katika mji wa pwani wa Saudi wa Jeddah yataandaa mkutano huo.

Katibu Mkuu wa OIC Hissein Brahim Taha alisema mkutano huo wa dharura unaonyesha namna nchi wanachama zilivyo na azma ya kutatua mgogoro ulioko Sudan.

Alisisitiza wito wake wa kusitishwa kwa kudumu kwa mapigano nchini Sudan na haja ya mazungumzo ili kulinda usalama, kulinda watu na kurejesha mchakato wa kisiasa.

Mapigano makali na makubwa kati ya vikosi vya jeshi la Sudan linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan, ambaye pia ni kiongozi wa nchi hiyo na wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Dharura (RSF) kinachoongozwa na Mohammad Hamdan Dagalo yalianza tokea tarehe 15 mwezi ulioisha wa Aprili kwenye maeneo mbalimbali ya Sudan na hasa katika mji mkuu Khartoum.

Mapigano hayo yangali yanaendelea na hadi sasa watu zaidi ya 500 wameshauawa licha ya pande hasimu kufikia mapatano ya kusitisha vita kwa muda huku kukiwa na taarifa kuhusu juhudi zinazoendelea za kusitisha mapigano hayo huko Sudan.  

Wapiganaji wa kikosi cha radiamali ya haraka (RSF) juzi Jumapili walitangaza kuwa watarefusha muda wa usitishaji mapigano nchini humo ili kuitikia na maombi ya kimataifa, kikanda na ya ndani. 

Umoja wa Mataifa umetabiri kuwa idadi ya wakimbizi huko Sudan itaongezeka na kupindukia watu 800,000 iwapo vita vitaendelea nchini humo. 

Watu walioshuhudia wameeleza kuwa ndege za kivita zinaruka katika anga ya mji wa Khartoum huku milio ya risasi ikisikika mara kwa mara. Wakati huo huo raia huko Sudan wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa mahitaji muhimu ya kama chakula, maji na dawa za matibabu.

3483397

 

Kishikizo: sudan oic
captcha