IQNA

Ibada ya Hija

Mahujaji Wasimama Arafat, Waomba Rahma ya Allah SWT

15:26 - July 08, 2022
Habari ID: 3475475
Mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu leo wamesimama katika uwanja wa Arafa hii, kisimamo hicho kikiashiria kilele cha ibada tukufu ya Hija.

Arafa ni jina la jangwa kubwa linalopakana na Mlima wa Jabalur Rahma ulioko kusini mashariki mwa Makka. Tangu adhuhuri ya siku hii Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu, al Kaaba, husimama katika uwanja wa Arafa na hadithi nyingi za Kiislamu zimetaja fadhila na utukufu mkubwa wa kisimamo hicho.

Katika siku hii ambayo huja kabla ya Siku Kuu ya Idul Adha, mahujaji  katika Mlima Arafat kuanzia mapema mchana hadi Magharibi katika ibada inayojulikana kama 'Wuquf Arafat'

Hadithi zinasema kuwa Mwenyezi Mungu SWT ameifanya ardhi ya Arafa ambayo ilikuwa medani ya matukio mengi muhimu ya kihistoria, kuwa mahala pa kuwapokea wageni wake wanaokwenda Hijja na ameweka meza na karamu yake pembeni ya Jabalur Rahma.

Magharibi ya siku hii ya leo Mahujaji wataondoka uwanja wa Arafa na kuelekea Mash'arul Haram na kujitayarisha kwa ajili na amali nyingine za Hijja, kama kulala Muzdalifa, na kufanya amali ya Jamarat (kumpiga shetani kwa mawe saba) Jumamosi.

Waislamu milioni moja wakiwemo raia wa kigeni 850,000 wamekusanyika katika mji mtakatifu wa Makka nchini Saudi Arabia kwa ajili ya Hijja ya mwaka huu, ikiashiria hatua kubwa kuelekea hali ya kawaida baada ya miaka miwili ya janga la corona ambapo idadi ya Mahujaji ilipunguzwa sana.

Hata hivyo idadi hii bado ni ndogo ikikumbukwa kuwa, kabla ya janga la corona Waislamu milioni 2.5 waliweza kutekeleza nguzo hiyo muhimu ya Uislamu  mwaka  2019.

Hija ni wajibu kwa kila Mwislamu mwenye uwezo lakini kutokana na gharama zinazozidi kuongezeka inamaanisha kuwa watu wengi mwaka huu hawawezi kuhiji hata baada ya kuweka akiba kwa miaka mingi.

Aidha matumaini ya raia wengi wa Ulaya na Marekani  Kuhiji mwaka huu yamefifia baada ya Saudi Arabia kuanzisha sheria hiyo mpya inayowalazimi wasafiri watarajiwa kutenga  nafasi kupitia tovuti ya serikali, mchakato ulioelezwa na wengine kuwa ni sawa na bahati nasibu.

4069359

Kishikizo: arafat ibada ya hija
captcha