IQNA

Saad Hariri ajiuzulu na kukiri kuwa hawezi kuunda serikali ya Lebanon

22:45 - July 15, 2021
Habari ID: 3474102
TEHRAN (IQNA)- Saada Hariri ambaye alikuwa na jukumu la kuunda serikali mpya ya Lebanon akiwa waziri mkuu kuunda serikali ameshindwa kufanya hivyo na sasa amejiuzulu.

Katika taarifa leo Alhamisi, Hariri amesema hajaweza kufanikiwa kuunda serikali ya Lebanon kutokana na hitilafu zilizopo.

Jana Hariri alimkabidhi Rais Michel Aoun orodha ya majina ya watu aliowapendekeza kuunda baraza lake la mawaziri.

Baada ya kukabidhi orodha hiyo kwa Aoun hapo jana, Saad Hariri alisema, kulingana na mpango uliopendekezwa na Ufaransa na ule uliopendekezwa na Spika wa Bunge la Lebanon Nabih Berri, serikali ijayo itakuwa na mawaziri 24 ambao watakuwa ni shakhsia wataalamu, yaani mateknokrati.

Hatahivyo Aoun amependekeza mabadiliko ya kimsingi katika orodha hiyo na hivyo Hariri amesema hawezi kuyatekeleza na kwa msingi huo amejiondoa katika mchakato wa kuunda serikali mpya ya Lebanon.

Hassan Diab ambaye anakaimu nafasi hiyo tokea alipojiuzulu mwezi Agosti mwaka jana kutokana na mlipuko katika bandari ya Beirut, ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuiokoa nchi yake wakati huu inapokabiliwa na mgogoro.

Lebanon ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa baada ya kutokea mlipuko huo mkubwa katika bandari ya Beirut. Mlipuko huo ulitokea tarehe nne Agosti mwaka jana na kusababisha vifo vya watu 190 na kujeruhi wengine 6,500.  Tokea wakati huo, makundi ya Lebanon yameshindwa kutatua hitilafu zao na kuunda serikali.

/3984345

Kishikizo: lebanon HARIRI diab aoun
captcha