IQNA

Iran yakanusha madai ya Marekani kuwa inawatumia silaha wanamgambo wa Taliban

22:35 - August 18, 2020
Habari ID: 3473081
TEHRAN (IQNA)- Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, matukio yanayojiri leo hii huko Afghanistan ni matokeo ya uingiliaji na uwashaji moto wa vita uliofanywa na Marekani ndani ya nchi hiyo.

Saeed Khatibzadeh, msemaji mpya wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa kauli hiyo kupinga tuhuma zisizo na msingi zilizotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani za kudai kwamba, Iran inalipelekea silaha kundi la Taliban la Afghanistan. Khatibzadeh amesisitiza kuwa: Yanayojiri leo hii nchini Afghanistan ni matokeo ya moto wa vita na uingiliaji wa Marekani katika masuala ya nchi hiyo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa: Tuhuma zilizotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ni aina mojawapo ya ubabaishaji wa kujivua na dhima na kujaribu kuzihadaa fikra za waliowengi ndani ya Afghanistan kuhusiana na misaada ya Washington kwa kundi la DAESH (ISIS) lililojipenyeza nchini humo.

Khatibzadeh amesema: Marekani bado haijatoa jibu kwa matakwa ya fikra za waliowengi kuhusu utambulisho wa helikopta zinazoruka kwenye eneo la anga ya Afghanistan linalodhibitiwa na shirika la kijeshi la NATO ambazo zinatumika kutoa misaada kwa Daesh.

Marekani na waitifaki wake ziliishambulia na kuivamia kijeshi Afghanistan mwaka 2001 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, lakini tangu wakati huo hadi sasa ugaidi, ukosefu wa amani na uzalishaji wa madawa ya kulevya vimekithiri mno ndani ya nchi hiyo.

3917025

captcha