IQNA

Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu yalaani mauaji ya Waislamu India

7:50 - March 13, 2020
Habari ID: 3472559
TEHRAN (IQNA) - Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu imelaani mauaji yanayofanywa ma Wahindu wenye misimamo mikali dhidi ya Waislamu nchini India na kuitaka serikali ya nchi hiyo isitishe mauaji na jinai hiyo.

Taarifa iliyotolewa Alhamisi na Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu, yenye makao yake mjini Tehran, imekemea ukandamiza wa haki za msingi na sheria zinazokanyaga haki za Waislamu milioni 200 wa India na kusema: Hatua hiyo haribifu imechukuliwa licha ya kwamba, kwa miaka mingi sasa Waislamu wa India wamekuwa wakiishi kwa amani na raia wenzao wenye ustaarabu na utamaduni wa siku nyingi. 

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, hatua za Marekani na Uzayuni wa kimataifa katika miaka ya hivi karibuni zinaonyesha kuwepo njama hatari dhidi ya Waislamu katika maeneo mbalimbali ya dunia hususan huko Palestina, Iraq, Syria, Yemen, Myanmar na sasa India. 

Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu imezitaka taasisi zote za kutetea haki za binadamu, wasomi na wanazuoni, viongozi wa nchi za Kiislamu, wapigania uhuru na nchi huru na zinazojitawala kuchukua msimamo imara, wa wazi na wa haraka wa kulaani inai hiyo na kutetea haki za Waislamu wa India kabla ya kutokea mauaji ya kimbari dhidi ya jamii hiyo. 

Baada ya  Bunge la India mnamo Disemba 11, 2019 kupitisha marekebisho ya sheria ya uraia inayowabagua Waislamu, Waislamu na wasio Waislamu nchini India wamekuwa wakiandamana kupinga sheria hiyo ya tata hususan mjini New Delhi ambapo makumi ya Waislamu wameuawa na maafisa usalama wakishirikiana na Wahindu wenye misimamo mikali.

Serikali ya India imefichua habari ya kuchomwa moto kikamilifu misikiti tisa na mamia ya nakala za Qur'an Tukufu katika hujuma zilizofanywa na Wahindu wenye misimamo mikali na chuki dhidi ya Waislamu.

Katika hujuma na mashambulizi hayo yaliyodumu kwa siku kadhaa, kwa akali Waislamu 50 wameuawa na wengine zaidi ya 400 wamejeruhiwa katiak hujuma hizo za kibaguzi na chuki.

3884925

captcha