IQNA

Watu Waliouawa India katika ghasia za India wapindukia 30 utawala wa Modi waendelea kukosolewa

11:31 - February 27, 2020
Habari ID: 3472511
TEHRAN (IQNA) - Idadi ya watu waliouawa katika ghasia zinazosababishwa na sheria tata yenye kuwabagua Waislamu katika mji mkuu wa India, New Delhi inazidi kuongeza ambapo takwimu mpya zinaonyesha kuwa, idadi hiyo imefikia 30 huku mamia ya watu wengine wakijeruhiwa.

Ripoti zaidi zinasema kuwa, machafuko hayo ya wapingaji na waungaji mkono wa sheria hiyo ya uraia iliyo dhidi ya Waislamu ambayo leo yameingia siku yake ya nne yameshuhudia pia misikiti kadhaa ikivamiwa na kuteketezwa kwa moto na makundi ya vijana wenye misimamo ya kibaguzi na chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Ghasia hizi zinatajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kuikumba India katika kipindi cha miongo kadhaa iliyopita, huku asasi za kijamii zikifanya pia maandamano ya amani ya kuitaka serikali iangalie upya sheria hiyo ya kibaguzi.

Sheria hiyo tata inaruhusu kupewa uraia wahajiri wasio Waislamu waliokimbilia India kutoka nchi jirani za Bangladesh, Pakistan na Afghanistan, huku ukiwanyima haki hiyo ya uraia Waislamu.

Sheria mpya ya uraia nchini India ambayo inaandaa mazingira ya kupatiwa uraia wahajiri wasiokuwa Waislamu, inalalamikiwa na jamii ya Waislamu nchini humo, asasi za kiraia na hata baadhi ya wanachama waandamizi wa chama tawala nchini humo cha Bharatiya Janata (JBP) ambao wanasema kuwa, sheria hiyo ni ya kibaguzi.

Wakati huo huo, serikali ya Narendra Modi, Waziri Mkuu wa India imeendelea kuandamwa na ukosoaji ndani na nje ya nchi hiyo kutokana na siasa zake zilizo dhidi ya Waislamu.

3881556

captcha