IQNA

Kauli mbiu ya Siku ya Misikiti Duniani

Misikiti, Mhimili wa Umoja wa Umma wa Kiislamu

14:16 - August 19, 2016
Habari ID: 3470532
Kauli mbiu ya Siku ya Kimataifa ya Misikiti mwaka hii imetajwa kuwa ni ‘Misikiti, Mhimili wa Umoja wa Ummah wa Kiislamu.

Akizungumza na IQNA, Hujjatul Islam Said Karami , Naibu Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu Iran anayeshughulikia maasuala ya Misikiti amesema Siku ya Kimataifa ya Misikiti itaadhimishwa Jumapili, Agosti 21.

Amesema katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Tehran, kutakuwa na harakati kadhaa za kuadhimisha siku hiyo ikiwa ni pamoja na kongamano la kimataifa.

Amesema misikiti zaidi ya 500 mjini Tehran itakuwa na maonyesho yenye yatakayohusu misikiti kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu.

Aidha amesema maimamu katika misikiti watatoa hotuba maalumu kuhusu tukio lililojiri katika Msikiti wa Al Aqsa huko Quds (Jerusalem) mnamo Agosti 21, 1969.

Kila mwaka, Waislamu kote duniani, mnamo Agosti 21 hukumbuka tukio la siku kama hii mwaka 1969 ambapo Mzayuni mwenye misimamo mikali waliteketeza mote eneo moja la Msikiti wa Al Aqsa na kuharibu Minbar ya Salahudin.

Moto huo uliwashwa na Mzayuni kutoka Australia aliyetumabuliwa kama Denis Michael Rohan ambaye alikuwa na itikadi potovu kuwa, kwa kuuteketeza Msikiti wa Al Aqsa angeharakisha kurejea Nabii Issa (Yesu) AS na kuandaa ujenzi wa hekalu ya Kiyahudi katika eneo hilo. Wakati huo maafisa wa Israel walitangaza kuwa mtu huyo aliyekuwa na uraia wa Australia, ni Mkisto mwendawazimu, lakini baadaye ilibainika kuwa Dennis ni Myahudi mwenye misimamo ya kuchupa mipaka na alichoma moto kibla hicho cha kwanza cha Waislamu kwa makusudi. Mbali na hayo ushahidi ulionesha kuwa Wazayuni wengine wenye misimamo mikali walimsaidia Michael Dennis katika harakati zake za kuchoma msikiti huo.

Quds na maeneo yake matakatifu yamekuwa yakishambuliwa na kuvunjiwa heshima tangu Wazayuni walipovamia na kukalia kwa mabavu ardhi ya Palestina. Katika kipindi chote cha miongo kadhaa iliyopita utawala wa kikatili wa Israel si tu kwamba hauwaonei huruma watoto wadogo na wanawake na umekuwa ukifanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, bali pia umekuwa ukivunja na kuhujumu misikiti na makanisa ya eneo hilo. Pamoja na hayo Msikiti wa al Aqsa ndio unaoshambuliwa na kuvunjiwa heshima zaidi kati ya maeneo yote matakatifu ya Palestina na hilo linafanyika ili kuuharibu kabisa msikiti huo na hatimaye kufuta kabisa utambulisho wa kihistoria wa Palestina. Utawala bandia wa Israel daima umekuwa ukilipa kipaumbele suala la kufuta utambulisho wa Kiislamu wa Quds tukufu na kuharibu maeneo matakatifu na ya kihistoria ya mji huo.

Israel hususan katika miongo miwili iliyopita ya mazungumzo na Wapalestina, imejenga majumba ya kamari, mahoteli, vituo vya anasa na maeneo ya ufuska kandokando ya Msikiti wa al Aqsa kwa shabaha ya kuuzingira msikiti huo. Vilevile utawala huo ghasibu unachimba njia za chini ya msikiti huo kwa lengo la kuuharibu.

Katika hali kama hiyo tangu kuasisiwa kwake, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikitetea haki za taifa linalokandamizwa la Palestina na kutahadharisha kuhusu matokeo na athari mbaya za kuharibiwa maeneo ya kale ya mji wa Baitul Muqaddas (Jerusalem). Iran pia imetoa wito wa kulindwa Quds na Palestina kama turathi ya Mitume wa Mwenyezi Mungu katika upeo wa kimataifa.

Misikiti, Mhimili wa Umoja wa Umma wa Kiislamu

3460740/

captcha