Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ambaye pia ni Amri Jeshi Mkuu wa Majeshi yote ya Iran amesema hayo Jumatatu mjini Tehran katika hafla ya kuapishwa na kupatiwa nishani wanachuo wahitimu wa mafunzo ya kijeshi katika Chuo Kikuu cha Kijeshi la Imam Hussein AS. Amesitiza kwamba, uistikbari na ubeberu umekasirishwa mno na hatua ya taifa la Iran ya kusimama kidete na kuongeza kwamba, licha ya kambi ya uistikbari kutumia kila wenzo na kufanya kila njama katika kipindi miaka 38 ili kuyasambaratisha Mapinduzi ya Kiislamu lakini umeshindwa kufikia lengo lake hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, hii leo mabeberu wanatumia kila wenzo, mashinikizo pamoja na njama za kiutamaduni, kiuchumi, kisiasa, propaganda pamoja na vibaraka wao wasaliti ili kuupigisha magoti mfumo wa Kiislamu hapa nchini na kuufanya ufuate matakwa yao; lakini wameshindwa kufikia lengo hilo na lililowakasirisha zaidi ni kuona taifa hili likiwa limesimama kidete na halitetereki na wananchi wake hawako tayari kuufuata uistikabari.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, kuzusha makelele kuhusiana na masuala kama ya nishati ya nyuklia, nguvu za makombora ya Iran na haki za binadamu hapa nchini ni visingizio tu na kusisitiza kwamba, sababu hasa ya uadui huu na huu uletaji visingizio ni hatua ya taifa hili ya kukataa katakakata kuwa mfuasi wa uistikbari.