IQNA

Wasiwasi kuhusu afya ya Sheikh Zakzaky

19:54 - April 12, 2016
Habari ID: 3470243
Mwanafunzi wa zamani wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, amebainisha wasiwasi wake kuhusu hali ya kiafya ya mwanazuoni huyo.

Katika mahojiano maalumu na IQNA, Mustafa Muhammad amesema wanachama kadhaa ya Harakati ya Kiislamu ya Nigeria IMN siku ya Ijumaa walikutana na Sheikh Zakzaky ambapo imebainika kuwa hali yake ya kiafya si nzuri.

Aidha amesema hali ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Nigeria ni mbaya kwani serikali inatekeleza njama maalumu za kuwakandamiza. Aidha amesema serikali ya Nigeria imechukua hatua za kuangamiza madhehebu ya Kishia nchini humo. Kwa mujibu wa Mustafa Muhammad, ambaye ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Kimatiafa cha Al Mustafa SAW mjini Qum, nchini Iran, serikali ya Nigeria inautazama Uislamu wa Kishia kuwa ni tishio katika nchi hiyo.

Wakati huo huo Mwanaharakati mmoja maarufu wa nchini Uingereza amekosoa vikali ukimya wa jamii ya kimataifa juu ya mauaji ya halaiki dhidi ya Waislamu nchini Nigeria.

Masoud Shajareh mkuu wa Tume ya Kiislamu ya Haki za Binadamu IHRC yenye makao yake London aliyasema hayo hapo Jumatatu katika mahojiano na kanali ya Press TV na kuongeza kuwa, ni miezi kadhaa sasa imepita tangu kujiri mauaji ya halaiki dhidi ya Waislamu nchini Nigeria ambapo hadi sasa ukatili huo haujachunguzwa. Shajareh ameongeza kuwa, ni suala la dharura kufuatiliwa wahusika wa jinai hizo na kupandishwa kizimbani.

Itakumbukwa kuwa mwezi Disemba mwaka jana jeshi la Nigeria lilishambulia kituo cha kidini cha Harakati ya Kiislamu ya Nigeria na kisha makazi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa harakati hiyo katika mji  wa Zaria kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Katika hujuma hiyo iliyojiri katika  jimbo la Kaduna, jeshi la Nigeria liliwaua Waislamu zaidi ya elfu moja katika eneo hilo na kisha kuizika miili ya wahanga hao katika kaburi la umati.

Aidha katika tukio hilo kiongozi wa Harakati ya Kiislamu Nigeria Sheikh Ibrahim Zakzaky alikamatwa pamoja na mke wake na hadi sasa wanashikiliwa katika jela za kuogofya za jeshi la nchi hiyo wakiwa na majereha na risasi mwilini.

3487484

captcha