IQNA

Mauaji ya Mashia nchini Nigeria

14:40 - December 14, 2015
Habari ID: 3463089
Vikosi vya jeshi la Nigeria Jumapili alfajiri vililvamia nyumba ya Sheikh Ibrahim Zakzaky Kiongozi wa Washia wa nchi hiyo katika mkoa wa Zaria jimboni Kaduna, na hatimaye kumtia mbaroni kiongozi huyo wa kidini.

Katika uvamizi huo, wanajeshi wa Nigeria waliwafyatulia risasi hadhirina waliokuwepo ndani ya nyumba ya Sheikh Zakzaky ambapo watu wengi waliuwa na wengine kujeruhiwa. Duru za habari zinasema kuwa watu wasiopungua 35 wameuawa kwenye uvamizi huo.
Vikosi vya jeshi la Nigeria vilimzingira Sheikh Ibrahim Zakzaky na magari ya deraya, lakini wafuasi na waungaji mkono wa kiongozi huyo wa Washia wa Nigeria waliunda ngao ya binadamu kwa kumzunguka kiongozi wao huyo ili kuvizuia vikosi vya Nigeria kuingia ndani ya nyumba yake. Tukio hilo lilijiri masaa kadhaa baada ya wanajeshi wa Nigeria kushambulia marasimu ya kidini katika Husseiniya ya Baqiatullah katika mji wa Zaria siku ya Jumamosi ambapo makumi ya Waislamu waliuawa. Baadhi ya duru zinadokeza kwa ujumla zaidi ya watu 100 wameuawa katika ukatili wa jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia.
Marasimu hayo yaandaliwa kwa ajili ya kuwakumbuka raia wa Nigeria wa madhehebu ya Shia ambao siku kadhaa zilizopita waliuawa katika shambulio lililofanywa na watu wenye silaha wasiofahamika. Washia wa Nigeria katika miji kadhaa nchini humo ukiwemo mji wa Katsina wamefanya maandamano kufuatia tukio hilo la leo la kuvamiwa nyumba ya Sheikh Ibrahim Zakzaky. Hata kama uvamizi huo wa Jumapili umenasibishwa kwa kundi la kigaidi la Boko Haram, lakini Washia wa Nigeria wanaamini kuwa, mamluki ndani ya jeshi la Nigeria wamehusika pia kwenye uvamizi huo. Jeshi la Nigeria limetekeleza shambulio hilo dhidi ya Waislamu wa Kishia na kiongozi wao nchini humo huku nchi hiyo ikiwa inakabiliwa na mawimbi ya mashambulizi ya kigaidi ya kundi la Boko Haram na kama wasemavyo weledi wa mambo, jeshi la Nigeria bado halijafanikiwa katika mapambano yake dhidi ya Boko Haram licha ya kutekeleza hatua kadhaa dhidi ya kundi hilo.
Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria alitangaza kuwa vipaumbele vyake vikuu ni kuliangamiza kundi la Boko Haram, lakini pamoja na hayo, kundi hilo la kigaidi lingali linaendeleza hujuma na mashambulizi yake nchini humo. Watu wasiopungua kumi waliuawa na wengine wengi pia kujeruhiwa kwenye mashambulizi ya jana ya Boko Haram karibu na kijiji cha Biu katika jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria. Aidha kundi hilo liliwafyatulia risasi raia karibu na kijii hicho, na kusababisha wenyeji wengi wa kijiji hicho kukimbia makazi yao. Duru za kieneo za Nigeria zimesisitiza kuwa, watu 11 wamejeruhiwa katika shambulio hilo la jana na wanamgambo wa Boko Haram wakiripotiwa kufanya uporaji na wizi katika nyumba za wakazi wa kijiji hicho. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, jeshi la Nigeria halina azma thabiti ya kuliangamiza kundi la Boko Haram na wanasema kwamba wakati mwingine jeshi la Nigeria hulitumia kundi hilo kama wenzo wa mashinikizo nchini humo.  Itakumbukwa kuwa, kundi la kigaidi la Boko Haram kitambo nyuma lilitishia kuwauwa Washia wa Nigeria ambapo katika mkanda wa video ulioutoa, Boko Haram ilitangaza kuwa Washia wa Nigeria wasubiri mashambulizi mengine dhidi yao. Watu wa madhehebu ya Shia kati ya milioni tatu hadi saba wanaishi Nigeria, huku kiongozi wao Sheikh Ibrahim Zakzaky akihesabiwa kuwa ni mmoja wa shakhsia muhimu na wenye taathira nchini humo. Ni zaidi ya miaka 30 sasa ambapo Sheikh Zakzaky anawaongoza Waislamu wa madhehebu ya Shia huko Nigeria. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, serikali ya sasa ya Nigeria haina lengo la kuwaangamiza Washia nchini humo, hata hivyo inavyoonekana ni kuwa ina wasiwasi na harakati za  Washia; na ili kudhamini usalama wa jamii ya watu hao na kukabiliana na vitendo vya kigaidi dhidi ya Washia nchini humo, serikali ya Nigeria si tu kuwa haifanya juhudi, bali wakati mwingine inajaribu kuchukua hatua pia katika uwanja huo. Kitendo kilichofanywa leo na jeshi la Nigeria pia, kinapasa kutathminiwa katika uwanja huo.

3462830

captcha