IQNA

Rais Rouhani

Uislamu ni dini ya amani, Iran itachangia vita dhidi ya ugaidi

12:25 - November 18, 2015
Habari ID: 3454175
Marais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Ufaransa wametangaza utayarifu wa nchi hizo mbili kwa ajili ya kushirikiana katika masuala ya usalama na habari za kipelelezi katika fremu ya mapambano dhidi ya ugaidi.

Rais Hassan Rouhani aliyasema Jumanne katika mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Ufaransa kuwa, lengo la magaidi ni kuwafanya watu wauchukie na kuuogopa Uislamu duniani na amesisitiza kwamba Iran ambayo ni mhanga mkubwa zaidi wa ugaidi iko tayari kushirikiana na Ufaransa katika masuala ya usalama na upelelezi katika mchakato wa kupambana na tatizo hilo. Rouhani ametilia mkazo suala la kuimarishwa mapambano dhidi ya ugaidi nchini Syria na kusema: Uislamu ni dini ya amani na unapinga aina zote za mashambulizi ya kigaidi. Amesema magaidi wanasema uongo pale wanapofanya jitihada za kujinasibisha na kujihusisha na Uislamu.
Rais wa Iran amesema suala la kuwatokomeza kabisa magaidi katika nchi za Syria na Iraq kama kipaumbele muhimu, linahitaji mashauriano na ushirikiano wa nchi zote na kusisitiza kuwa, Iran inatoa wito wa kuanzishwa kambi yenye umoja kwa ajili ya kupambana na ugaidi kote duniani.
Rais Rouhani ametoa tena mkono wa pole kwa taifa na serikali ya Ufaransa kutokana na mauaji ya raia wa nchi hiyo katika mahambulizi ya kigaidi ya hivi karibuni mjini Paris na kusema: Nchi zinazotumia ugaidi kama wenzo wa kutimiza maslahi yao zinapazwa kutambua hatari ya hatua kama hizo kwa dunia nzima.
Kwa upande wake Rais François Hollande wa Ufaransa amesema kipaumbele cha kwanza kwa sasa ni kupambana na ugaidi katika nchi za Syria na Iraq na amesisitiza udharura wa kutokomezwa vyanzo vya fedha na silaha vya makundi ya kigaidi.

Zaidi  ya watu 130 waliuawa Ijumaa usiku wakati magaidi wa kundi la Wakufurishaji wa Daesh au ISIS waliposhambulia maeneo kadhaa ya Paris, Ufaransa.

Magaidi wa ISIS wanaeneza chuki dhidi ya Uislamu

Wakati huo huo Rouhani amesema wimbi la mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa hivi sasa na kundi la kigaidi na kitakfiri la ISIS au Daesh katika maeneo tofauti ya dunia yanadhamiria kuzidisha chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu ulimwenguni. Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa: “Uislamu ni dini ya huruma na amani, na kwamba mashambulizi ya hivi sasa ya ISIS hayafai kuruhusiwa kuendelea kwa kuwa yanazidi kupalilia mbegu za chuki na uhasama dhidi ya Waislamu duniani, na hususan katika nchi za Ulaya na Marekani.” Rais wa Iran amekariri kuwa Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kupiga vita harakati zote za kigaidi huku akitoa wito kwa jamii ya kimataifa kushirikiana kuzima jinamizi la ugaidi, ambalo limesababisha wanawake, watoto na raia wasio na hatia kupoteza maisha yao. Katika mazungumzo yake ya simu na Rais wa Ufaransa hapo jana, Rais Rouhani alisema suala la kuwatokomeza kabisa magaidi linahitaji mashauriano na ushirikiano wa nchi zote na kusisitiza kuwa, Iran inatoa wito wa kuanzishwa kambi yenye umoja kwa ajili ya kupambana na ugaidi kote duniani.

3453779

captcha