IQNA

Kuzaliwa Nabii Isa AS kwa mtazamo wa Qur'ani Tukufu

20:12 - December 27, 2014
4
Habari ID: 2638287
Hivi Wakristo duniani wanaadhimisha siku ya kuzaliwa Nabii Isa AS. Mamia ya mamilioni ya Wakristo duniani katika makundi yao tofauti wanaadhimisha kuzaliwa Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu, rehema za Allah ziwe juu yake na mama yake mtoharifu.

Isa bin Maryam ni Mtume mkubwa na mtukufu wa Allah. Kwa mujibu wa mapokezi ya Wakristo, Nabii huyo wa Allah alizaliwa tarehe 25 Disemba huko Baytul Lahm, Palestina. Tab'an hakuna ushahidi wa kutosha wa kuthibitisha kuwa Nabii Isa AS alizaliwa tarehe 25 Disemba na ndio maana baadhi ya makundi ya Wakristo yanaamini kuwa Nabii Isa AS alizaliwa tarehe 6 Januari. Wakristo wa Orthodox kama vile wa nchini Ethiopia wao wanaamini kuwa Nabii Isa AS alizaliwa tarehe 7 Januari na ndio wakati wa sherehe zao za X-Mass. Katika sehemu moja ya maandishi yake, kitabu cha Kikristo cha Misingi ya Biblia kimeandika: "Kosa lingine kubwa la Ukristo wa watu wengi ni kuhusu siku ya kuzaliwa Yesu. Wachungaji walikuwa wamelala kondeni na mifugo yao wakati wa kuzaliwa Kristo (Luka 2:8)." Kitabu hicho cha masomo ya Kikristo cha Misingi ya Biblia kinasema, wachungaji wasingeweza kulala nje kondeni tarehe 25 Disemba inayodaiwa kuzaliwa Nabii Isa AS kwani ni kipindi cha baridi kali na watu hawawezi kulala nje kondeni kipindi hicho. Pia kimeandika: "Kristo (wakikusudia Nabii Isa AS) aliishi miaka 331 au 332 na kisha alikufa kwenye sikukuu ya Pasaka, basi inapasa kuwa alizaliwa miezi sita upande mwingine wa Pasaka, yaani karibu mwezi wa September/October." Kimeandika: "Tarehe 25 Disemba ilikuwa ni sikukuu ya Kipagani huko Ulaya kabla ya Ukristo kuingia. Kwa sababu hiyo Wakristo wa kweli wasisherehekee kuzaliwa kwa Kristo tarehe 25 Disemba. Kwa matendo, waumini wa kweli wa Kristo watumie siku za mapumziko ya watu wote, k.m Krisimasi, kuabudu pamoja popote iwezekanavyo."

Nabii Isa AS alizaliwa kwa njia za muujiza kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Alizaliwa bila ya baba na mama mtoharifu ambaye hakupata kukutana kimwili na mwanamme yeyote. Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu alikuwa na miujiza mengi. Alipewa Utume akiwa bado mchanga na alizungumza akiwa ndani ya kisusu cha watoto wachanga tena hakuzungumza maneno ya ovyo, bali maneno matukufu. Katika sehemu moja ya aya zinazoelezea namna alivyozaliwa Mtume huyo mtukufu, Qur'ani Tukufu inasema katika Surat Maryam aya za 29 na 30 kwamba: "(Maryam) akawaashiria (mtoto). Wakasema: Vipi tumsemeze aliye bado mdogo yumo katika mlezi (yaani kisusu cha watoto wachanga). (Nabii Isa akasema): Hakika mimi ni mja wa Allah. Amenipa Kitabu na amenijaaliwa kuwa Nabii." Vile vile Mtume huyo wa Allah anasema katika sura ya Aal Imran aya ya 49 kwamba: "Na ni Mtume kwa Wana wa Israili kuwaambia: Mimi nimekujieni na Ishara kutoka kwa Mola Mlezi wenu, ya kwamba nakuundieni kwa udongo kama sura ya ndege. Kisha nampuliza anakuwa ndege kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na ninawaponesha vipofu wa tangu kuzaliwa na wakoma, na ninawafufua maiti kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na ninakwambieni mnachokila na mnachoweka akiba katika nyumba zenu. Hakika katika haya ipo Ishara kwenu ikiwa nyinyi ni wenye kuamini."
Nabii Isa AS alikuja kutilia nguvu mafundisho ya Taurati ya Nabii Musa AS. Tab'an katika baadhi ya mambo aliamrishwa na Mwenyezi Mungu kufuta sheria alizokuja nazo Nabii Musa AS. Katika aya ya 63 ya Surat Zukhruf, Qur'ani Tukufu inasema: "Na alipokuja Isa na dalili zilizo wazi, alisema: Nimekujieni na hikima, na ili nikuelezeni baadhi ya yale mliyokhitalifiana. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na mnit'ii mimi." Yaani alikuja na hikima na mafundisho mapya, na pia kuwafafanulia Banii Israel yale waliyokhitalifiana katika mafundisho ya Nabii Musa AS. Aidha katika Surat as Saf aya ya 6 tunasoma: "Na Isa bin Mariamu aliposema: Enyi Wana wa Israili! Hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, ninayethibitisha yaliyokuwa kabla yangu katika Taurati, na mwenye kubashiria kuja Mtume atakaye kuja baada yangu; jina lake ni Ahmad! Lakini alipowaletea hoja zilizo wazi, walisema: Huu ni uchawi ulio dhaahiri!" Nabii Isa AS alifanya kazi kubwa ya kuwalingania wana wa Israili mafundisho ya Mwenyezi Mungu na kujibu maswali yao na kuonyesha miujiza mingi, hata hivyo, Mayahudi walikuwa wagumu mno kumwamini. Hadi alipokata tamaa nao, aliamua kuteua wanafunzi wake maalumu kati ya wale wachache waliomuamini ili wamsaidie katika kufikisha mafundisho ya Mwenyezi Mungu. Mayahudi walishindwa kuvumilia mafundisho ya Mtume huyo wa Allah yaliyosimama juu ya hoja madhubuti na kuamua kufanya njama za kumuua mtukufu huyo.
Hata hivyo, wakati wakuu wa Kiyahudi walipoamua kwenda kumuua Nabii Isa AS Mwenyezi Mungu alimuokoa mja wake huyo na kumpaisha mbinguni na akamfananisha mmoja wa Mayahudi kwa sura ya Nabii Isa AS. Hadithi mbalimbali za Bwana Mtume Muhammad SAW zinasema kuwa Nabii Isa AS atarejea duniani wakati wa kudhihiri Imam Mahdi AS na atasali na Waislamu pamoja na Imam Mahdi AS. Jina la Isa AS limetajwa mara 45 katika sura 13 tofauti za Qur'ani Tukufu. Hata hivyo, kupaishwa mbinguni Nabii Isa AS ulikuwa mwanzo wa kupotoshwa na kuingizwa mambo yasiyo sahihi katika mafundisho ya Nabii huyo wa Mwenyezi Mungu. Ukandamizaji dhidi ya wafuasi wa kweli wa Masih Isa AS yaliongezeka mno kutokana na kuwa maadui wa Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu walishindwa kujibu hoja zake zilizo wazi ambazo zilikuwa vigumu kuvunjwa. Wafuasi wa Nabii Isa AS walikuwa wanadhulumiwa sana na Mayahudi na Warumi. Wanahistoria wanasema kuwa, ukandamizaji huo ulipelekea kuingizwa fikra za kipagani katika mafundisho ya Mtume huyo wa Allah. Moja ya fikra hizo za kipagani ni kudai kuwa Masih Isa ni mwana wa Mungu. Fikra ya Utatu nayo ni miongoni mwa upotoshaji mkuu ulioingizwa kwenye mafundisho ya Nabii Isa AS. Fikra hiyo inamgawa Mwenyezi Mungu katika sehemu tatu, mungu baba, mungu mwana na mungu roho mtakatifu. Imani hiyo inajikanganya yenyewe kwani waliopandikiza imani hiyo ndani ya mafundisho ya Nabii Isa AS wanadai kuwa, miungu wote hao watatu, ni mmoja. Kudai kuwa miungu hao watatu ni mungu mmoja kumezidi kuifanya fikra ya Utatu iwe muhali kueleweka na kukubaliwa na watu wenye akili. Kwa hakika haiingiliki akilini moja kuwa tatu na tatu kuwa moja. Qur'ani Tukufu imekataza mno suala la kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kumuingiza kwenye Utatu. Mwenyezi Mungu anasema wamekufuru wanaosema kuwa Hakika ya Mwenyezi Mungu ni Mmoja wa miungu hao watatu. Vile vile Qur'ani Tukufu inasema kwamba siku ya malipo, Mwenyezi Mungu atamuuliza Mtume Wake Isa AS, je, ni wewe uliyewaambia watu wakufanye wewe na mama yako miungu wawili. Nabii Isa atawakana vikali watu hao wanaosema yeye ni Mungu au mwana wa Mungu au sehemu ya Mungu, kama isemavyo fikra potofu ya Utatu.

uingizwa upotofu ndani ya mafundisho ya Nabii Isa AS kulikita mizizi zaidi katika karne za kati yaani karne za giza barani Ulaya. Viongozi wa Kanisa walichukulia maendeleo yote ya kidunia kama vile fikra ya kwamba dunia ni sayari inayozunguka kuwa ni ukafiri na walimuhukumu kifo kila mtu aliyekuwa na fikra kama hizo. Viongozi hao wa Kanisa walishirikiana pia na wafalme madikteta kuua maelfu ya watu kwa kutekeleza adhabu za kikatili za kutumia zana za kukatia vichwa za guillotine (gelotin) kwa sababu tu watu hao walitofautiana na Kanisa katika kuelewa mafundisho ya Nabii Isa AS. Ukandamizaji huo wa Kanisa katika kipindi cha karne za kiza ulidumu miaka elfu moja. Watu walishindwa kuvumilia dhulma na muda wote huo kulifanyika njia mbalimbali za kupambana na ukatili huo. Ni kwa sababu ya ukatili huo wa viongozi wa Kanisa na upotofu ulioingizwa kwenye mafundisho ya Nabii Isa AS ndio maana katika karne ya 15 Milaadia kwenye kipindi cha Renaissance, watu wa Ulaya wakalitenga kabisa Kanisa katika maisha ya watu. Ni vitendo hivyo vya viongozi wa Kanisa na pia upotofu ulioingizwa kwenye mafundisho ya Masih AS ndio maana zilipata nguvu fikra za kuitenganisha dini na maisha ya watu na hivyo kukajitokeza pia fikra za kisekula, za kupinga kikamilifu dini na hadi leo hii fikra ya kutenganishwa dini na maisha ya kijamii na kisiasa ya watu bado zipo na zina nguvu. Mafundisho makubwa ya Nabii Isa AS yalikuwa ni kumwabudu Mungu Mmoja Ambaye pia Ndiye Mungu wake yeye, kueneza mapenzi baina ya watu na kujiepusha na vita na uhasama. Hata hivyo mauaji makubwa zaidi yaliyoripotiwa katika historia ya mwanadamu hasa yale ya karne za 18 na 19 Milaadia yamefanywa na Wakristo ambao wanadai ni wafuasi wa Nabii wa upendo na amani, Masih Isa AS. Wakoloni wa Ulaya ambao wamefanya ukatili na dhulma kubwa katika nchi mbalimbali duniani hasa za Afrika wanadai ni wafuasi wa Yesu, yaani Masih Isa AS. Kuuliwa kinyama Waafrika, kuangamizwa kizazi cha Wahindi wekundu katika bara la Amerika, vita vya kwanza na vya pili vya dunia, ukatili wa makaburu huko Afrika Kusini, ubeberu mkubwa unaoendelea hivi sasa katika sehemu mbalimbali za dunia ni sehemu ndogo tu ya jinai za watu wanaodai ni wafuasi wa Nabii Isa AS.
Hivi sasa pia mafundisho matukufu ya Masih Isa AS yanatoweka kwa nguvu katika nchi za Ulaya na Marekani zinazodai kuwa wafuasi wa Mtume huyo wa Allah. Nchi hizo hivi sasa zimezama kwenye migogoro wa kimaadili na kimaanawi. Nguzo ya kifamilia imedhoofika mno katika nchi hizo licha ya kwamba kulinda nguzo ya familia ndicho kitu kinachosisitiziwa mno na dini zote. Hivi sasa vitendo mbalimbali za kifuska kama vile maingiliano ya watu wa jinsia moja, kutembea uchi, kubadilisha jinsia za watu, ulawiti na uchafu mwingine unaofanywa na viongozi wa Kanisa ni mambo ambayo yameenea sana katika nchi za Ulaya na Marekani. Kiwango cha talaka kimeongezeka mno na ripoti zinasema kuwa, katika baadhi ya nchi za Magharibi kama zile za Scandinavia, asilimia hadi 80 ya watoto wanazaliwa nje ya ndoa. Idadi ya watoto wanaolelewa na mzazi mmoja imeongezeka sana. Watu wanaokwenda Kanisani siku za Jumapili imepungua mno. Fikra za kilahidi na kukanusha dini zimepata nguvu sana katika jamii za nchi hizo, huku kumvunjia heshima Mtume wa Allah, Nabii Isa AS likiwa ni jambo la kawaida kabisa katika nchi hizo. Tab'an hatuwezi kufumbia macho mchango uliotolewa na kasfa za ulawiti, ubadhirifu wa fedha, kukubali baadhi ya makanisa viongozi wanaojamiiana watu wa jinsia moja n.k, katika mambo hayo.
Alaakullihaal, watu wanaojinasibisha na Nabii Isa AS yaani Wakristo wanaiadhimisha X-Mass kwa shauku na ufanisi mkubwa. Hiyo inahesabiwa kuwa ndiyo sherehe kubwa zaidi kwao. Hata hivyo inasikitisha kuona kuwa mafundisho matukufu ya Nabii Isa AS yaani kumwabudu Mungu Mmoja bila ya kumshirikisha na chochote, uadilifu, mapenzi na amani; yanazidi kufifia katika jamii za watu hao.../mh

2636098
 

Imechapishwa: 4
Inatathminiwa: 0
Haiwezi kuchapishwa: 1
Omar Aliy Bakar
1
1
Tunashukuru sana kwa mafundisho haya matukufu, hakika allah atakulipa hapa duniani na akhera pia, Ahsante sana na mungu akujaze kheri na maisha marefu na yenye baraka na manufaa kwako.
Bila jina
2
0
Tujitahd Kusom Vtab Ili Tuwez Kufanya Yampendzayo Mwnyzimung
Hassan Al Mutwafi
0
2
Jazakllah khair
Bila jina
0
0
Safi sana kwa makala hii makafiri bila xhaka wanaelewa taratibu
captcha