IQNA

Mantiki ya kubaathiwa Mtume Mtukufu SAW

16:58 - May 27, 2014
Habari ID: 1411465
Tarehe 27 Rajab Mwaka wa Tembo na akiwa na umri wa miaka 40, Mtume Muhammad (SAW) alikuwa juu ya kilele cha Mlima Hira, akijishughulisha na ibada ndani ya pango la mlima huo, ambapo ghafla malaika Jibril AS alimteremkia huku akiwa amebeba wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu SW.

Malaika Jibril alikuwa amebeba ujumbe wa bishara ya utume kwa Mtume Mtukufu (SAW), ambapo alianza kumsomea aya za mwanzoni za Surat 'Alaq zinazosema: "Soma kwa jina la Mola wako aliyeumba. Amemuumba Mwanadamu katika pande la damu. Soma, na Mola wako ni Mtukufu mno. Ambaye amefunza (kuandika) kwa kalamu. Amemfunza mwanadamu asilolijua." Kwa utaratibu huo, wahyi na utume, vikawa vimeanza kwa jina la Mwenyezi Mungu na kusoma kwa kalamu, yaani mafundisho yaliyojumuisha tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Wapenzi wasikilizaji, huku tukikupeni mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa kuwadia siku hii tukufu ya kubaathiwa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW), Mtume wa rehema, tunakuombeni mjiunge nasi hadi mwisho wa kipindi hiki maalumu tulichowaandalieni kwa mnasaba huu adhimu
Kubaathiwa kuna maana ya kusimama na kuwa tayari kwa ajili ya kutenda kazi fulani. Na siku ya 'Mab'ath ni siku ambayo, Mtume wa Uislamu Muhammad (SAW), alipewa rasmi Utume. Kutumwa Mtume (SAW) ulikuwa mwanzo wa kumuokoa mwanadamu kutokana na shirki, kutenda vitendo vilivyo kinyume na uadilifu, ubaguzi, ujinga na ufisadi na kumuongoza kwenye tawhidi, umaanawi, uadilifu na utukufu. Aidha kubaathiwa, kuliambatana na kuanza mwamko wa kimaanawi na kuleta mapinduzi katika ulimwengu wa mwanadamu, mapinduzi ambayo athari zake bado zinaendelea kushuhudiwa hadi leo. Mabadiliko haya ya kiroho, yaliwaongoza wanadamu waliokuwa wakiabudu masanamu na kuwaelekeza kwenye chimbuko la maumbile na kuwaonya dhidi ya kufanya matendo machafu, huku yakiwataka wafanye matendo mema. Siku ya kubaathiwa Mtume Muhammad (SAW), ulikuwa ni mwanzo wa kumuondoa mwanadamu kutoka katika giza kuelekea kwenye nuru. Ni kwa ajili hiyo ndipo Imam Khomeini (MA) akaitaja siku hiyo ya kubaathiwa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) kuwa ni siku tukufu zaidi ulimwenguni. Kwa mtazamo wa Imam Khomeini, siku ya kubaathiwa Mtume wa Mwisho (SAW), hailinganishwi na siku nyingine yoyote ile. Imam Khomeini amesisitizia kuhusiana na suala hilo kwa kusema kuwa, siku ya kubaathiwa Mtume Muhammad SAW ni siku kubwa ambayo haina mfano wake na wala hapatatokea siku nyingine kama hiyo katika mustakbali. Ni siku ya kubaathiwa Mtume aliyediriki daraja zote za kinafsi na za mbinguni, na akafahamu sheria zote za dhahiri na batini. Kwa ajili hiyo, hakuna haja ya kutumwa ujumbe au Mtume mwingine baada yake.
Kubaathiwa Mtume Mtukufu SAW, kwa hakika yalikuwa majaaliwa katika historia. Tukio hilo kubwa limebainishwa kwenye aya tukufu aliyoteremshiwa Mtume Mtukufu na kulieleza tukio hilo kuwa ni neema kubwa. Mwenyezi Mungu mtukufu anasema hivi katika aya ya 164 ya Surat Aal Imraan:  'Hakika Mwenyezi Mungu amewaneemesha waumini kwa kuwaletea Mtume miongoni mwao, anayewasomea Aya zake ma anayewatakasa na kuwafundisha Kitabu na hekima. Na hakika kabla ya hapo walikuwa katika upotofu wa dhahiri'. Kubaathiwa Mtume SAW tunaweza kukutaja kuwa ni kufunguliwa ukurasa mpya katika historia ya mwanadamu, ambapo pia tunaweza kulitaja tukio hilo kuwa ni mapinduzi makubwa yaliyotokea ulimwenguni. Ni vyema kuelewa na kufahamu hali iliyotawala katika zama zile za wakati wa kukaribia kubaathiwa  Mtume Mtukufu SAW na adhama ya ujumbe wake huo. Kabla ya kubaathiwa Mtume SAW ulimwengu uligubikwa na migogoro na mtenguko wa maadili. Ujinga, uporaji, dhuluma na ukandamizaji wa haki za wanyonge na masikini, ufisadi uliochupa mipaka, ubaguzi na vitendo vingine vichafu vilivyokuwa mbali na maadili na ubinadamu, viliigubika jamii ya mwanadamu katika zama hizo. Katika maeneo yote, eneo la Bara Arabu na hasa katika mji wa Makka kulikuwa na hali mbaya zaidi ya kiutamaduni, kisiasa, kiuchumi, kijamii na isiyo ya kibinadamu. Heshima ya Waarabu katika zama za ujahiliya huko Makka ilikuwa ni kuyaabudu, kuyataradhia na kuyaomba msaada  masanamu yaliyochongwa kwa kutumia miti mikavu, ambapo  mtu yeyote mwenye akili, ufahamu na uelewa alishangazwa na kusikitishwa na kitendo hicho.
Mwenyezi Mungu SW ameashiria kwenye aya nyingi za Qurani Tukufu baadhi ya mila chafu za kijahiliya na zisizo za kibinadamu na kuwataka watu wajiweke mbali na mila hizo potovu na batili zilizokuwa zimeshika kasi katika zama hizo za ujahiliya. Kuna riwaya inayoelezea hali iliyokuwa ikitawala wakati huo huko Saudi Arabia wakati wa kukaribia kubaathiwa Mtume Mtukufu SAW kwa kusema: 'Siku moja Qays bin 'Aswim alikwenda kwa Mtume Mtukufu SAW na kumuambia; Ewe Mtume wa Allah!, Mimi niliwazika wakiwa hai  binti zangu wanane  wakati wa zama za ujahilia. Wakati Qays alipokuwa akimueleza Mtume kisa cha kuwazika binti zake wanane wakiwa hai, Mtume aliathirika mno; kwa kadri kwamba mwili wake ulisisimka na kububujika machozi kutokana na jinsi alivyoathiriwa na kisa hicho na kusema; hiki ni kitendo cha kikatili mno na mtu yeyote katili na asiye na huruma hatopata rehema za Mwenyezi Mungu'.
Huenda katika siku hizo hakuna sehemu yoyote ulimwengu iliyokuwa ikiamini hurafa, uchupaji mipaka na ufisadi wa kijamii mithili ya eneo la Saudi Arabia. Waarabu katika zama hizo licha ya kutojua kusoma na kuandika, mitazamo yao pia ilikuwa mbali na mantiki na akili na walikuwa wakifuata na kukumbatia mila, desturi na hurafa zisizo na msingi. Mtume Mtukufu SAW alitumwa na kupewa ujumbe kwa lengo la kuwaongoza watu waliopotea sio wale tu walioko Bara Arabu , bali kuwaongoza  na kuwaokoa watu wote ulimwengu. Ujumbe wa Mtume Mtukufu SAW unaonyesha wazi kwamba ulinganio wake tokea mwanzo ulikuwa umejikita kwenye misingi ya kiakili, kimantiki na dalili. Qurani Tukufu na Mtume Mtukufu SAW wanawataka watu wote kufuata na kukubali kile ambacho kinakubaliana na akili zao.
Miongoni mwa watu walioishi katika zama za Mtume SAW walikuwepo baadhi ambao hurafa ilikuwa sehemu ya maisha yao, lakini Mtume Mtukufu aliweza kupambana na fikra hizo. Kwani fikra za tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu, ni kupambana na ujahili, hurafa na mambo mengine yasiyotumia mantiki. Bila shaka moja kati ya malengo ya Mtume Mtukufu, ilikuwa ni kupambana na hurafa na kuweka wazi mambo ya kiakili na kimantiki. Mtume Muhammad SAW kwa nguvu zake zote alifanya juhudi za kuhakikisha kwamba watu wanafuata uhakika na wala sio vitendo ya kihurafa. Imenukuliwa kwenye tarikh na historia kwamba, wakati alipofariki dunia mwana pekee wa kiume wa Mtume Muhammad SAW aitwaye Ibrahim; Mtume Mtukufu alilia mno kutokana na kifo hicho.  Siku aliyofariki dunia mwana wa Mtume kulitokea tukio la kupatwa jua, na baadhi ya watu waliokuwa wanaamini mambo ya hurafa walisema kwamba, tukio hilo lilionyesha adhama ya msiba huo na wakasisitiza kwamba jua lilipatwa kutokana na kifo cha mtoto wa Mtume Mtukufu SAW. Wakati Mtume Muhammad SAW aliposikia maneno hayo; alipanda juu ya mimbari na kusema, 'mwezi na jua ni alama mbili kubwa zinaoonyesha nguvu zisizokuwa na ukomo za Allah SW na kamwe tukio hili halihusiani na kifo au uhai wa mtu yeyote'. Ijapokuwa angeliweza kulifungamanisha zaidi tukio hilo na ujumbe wake na itikadi za watu; lakini mtukufu huyo kamwe hakuwa tayari kuimarisha nafasi yake katika nyoyo za watu kwa kutumia njia za hurafa. Mtume Mtukufu SAW hakutaka kutumia udhaifu waliokuwa nao watu wa zama zile likiwemo suala la itikadi na mambo ya hurafa ili aweze kuitumia fursa hiyo kwa kuwaongoza watu, bali alitaka watu waingie katika dini ya Kiislamu wakiwa na uelewa, elimu na maarifa sahihi ya dini hiyo. Kwani Mwenyezi Mungu amesema katika Qurani Tukufu kwamba; Uwalinganie watu  kwenye njia ya Mwenyezi Mungu kwa hekima na mawaidha mazuri. Kufikiri na kutaamali ni miongoni mwa masuala ambayo yalisisitizwa na kutiliwa mkazo mno na Mtume Mtukufu SAW. Mtukufu Mtume Muhammad SAW amesema; 'Mwenyezi Mungu SW hakumpa mja Wake kitu bora zaidi kuliko akili'.  Kimsingi tunapaswa kutegemea zaidi akili katika masuala ya kiitikadi na katika kila mfumo wa kifikra. Iwapo tunataka kuthibitisha tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu, kuwepo Mtume, Wahyi na masuala mengine mithili ya hayo, tunapaswa kutumia zaidi dalili za kiakili. Akili pekee ndiyo inayoweza kumsaidia mwanadamu iwapo anataka kuainisha itikadi na imani sahihi na isiyokuwa sahihi na akili pia ndiyo inayoainisha mipaka baina ya haki na hurafa. Marehemu Allamah Sayyid Tabatabai mmoja kati ya wasomi wakubwa hapa nchini ameeleza kuhusiana na umuhimu wa nafasi ya akili katika mafunzo ya Qurani Tukufu kwa kusema: 'Kama tutachunguza na kuzingatia kwa makini aya zilizomo ndani ya Qurani Tukufu, tunaweza kuona zaidi ya aya mia moja zinazowataka watu wafikiri na kutumia mantiki na zinazotubainishia kwamba Mtume SAW alikuwa akitoa dalili za kuthibitisha haki na kutokomeza batili. Mwenyezi Mungu hakuteremsha hata aya moja ndani ya Qurani Tukufu anayomuamrisha mja Wake aamini na kufuata jambo kibubusa bila ya kufahamu uhakika wake. Mtume Mtukufu Muhammad SAW amewasisitizia sana Waislamu juu ya suala la kutafuta elimu, hata kama itakuwa katika nchi za mbali, kama vile ardhi ya Uchina. Mtume Mtukufu alikuwa akitoa msisitizo mkubwa katika masuala ya kutafuta elimu na hata imenukuliwa akisema kwamba, katika moja ya vita vilivyopiganwa katika zama zake, Mtume alitoa pendekezo la kuachiliwa huru mateka wa kishirikina wanaojua kusoma na kuandika kwa sharti wawafundishe Waislamu ambao walikuwa bado hawajapata neema ya kujua kusoma na kuandika. Jambo la kushangaza na kusikitisha hapa ni hili kwamba leo hii baadhi ya watu wenye fikra potovu kwa kutumia jina la Uislamu na kwa kisingizio cha kuhuisha suna za Mtume Mtukufu SAW wanawashambulia wanafunzi na baadhi ya vituo vya elimu kwa kutumia jina la Uislamu. Hivi karibuni kumeshuhudiwa kundi la Boko Haram la nchini Nigeria likiwateka nyara wanafunzi wasichana wasiopungua 250 wanaosoma katika shule ya sekondari katika jimbo la Borno lililoko kaskazini mashariki mwa Nigeria. Swali la kujiuliza hapa ni hili kwamba, je, ni akili gani inayoweza kukubali kufanyika vitendo kama hivyo na kuvinasibisha na Uislamu na suna ya Mtume Muhammad SAW? Tukio hilo ni la kusikitisha mno, kwani licha ya kuuchafua Uislamu, linaonyesha kwamba wahusika wa vitendo hivyo hawajui kitu kuhusiana na misingi ya dini ya Kiislamu. Waislamu wanaamini kwamba Mitume wote walifanya juhudi bila ya ukomo kwenye kipindi chote cha maisha yao ili kuwapatia saada na ufanisi watu wote na kujiweka mbali na ujinga. Mitume hao walikuwa wakiwalingania watu kwenye misingi ya tauhidi na kumpewekesha Mwenyezi Mungu na kujiondoa kwenye makucha ya fikra za hurafa na badala yake walikuwa wakiwalingania kwenye uhuru na kufanya juhudi za kufikia daraja la  uadilifu, kupambana na utumwa, udhalimu na kuwaunga mkono watu waliodhulumiwa na wanyonge. Viongozi hao wa kidini walikuwa wakiwashawishi watu wajitafutie elimu na kuzingatia utukufu wa mwanadamu na thamani za kimaadili, kwani hayo ni miongoni mwa mafundisho makuu ya Mtume Mtukufu SAW, ambayo yalikuwa na thamani kubwa kwa madola ya Kiislamu na jamii nyingine za mwanadamu.
Tazkiya ambayo ndio lengo kuu la kubaathiwa Mtukufu Mtume (SAW), ina maana ya kuondoka katika kiza la nafsi na kupambana na matamanio na vishawishi vyote vya ndani kwa ajili ya kuingia katika anga ya usafi wa kimaanawi. Chanzo cha tofauti na migogoro yote ambayo inashuhudiwa leo katika jamii ya mwanadamu, kinatokana na upinzani ambao unapatikana katika nafsi za wanadamu. Chanzo cha kuchupa mipaka na kuzuka tofauti kati ya wanadamu, hutokana na nafsi za wanadamu kutotosheka wala kukinai. Kwa hakika suala hilo, hupatikana katika matabaka yote ya watu, wakiwemo wafanyakazi, watu wa vijijini na hata viongozi wenye madaraka ya juu. Hakuna shaka kwamba, kukosekana utakaso wa nafsi kwa viongozi, ni jambo lenye hatari kubwa. Kuhusiana na suala hilo, Imam Khomeini MA anasema: "Ikiwa watu wa kawaida hawatajitakasa na wakafanya maovu, madhara ya uovu wao huwa na ukomo maalumu. Ikiwa mtu mmoja atafanya uovu sokoni au katika kijiji, inawezekana uovu huo ukawa na athari kwa kiasi fulani tu, lakini ikiwa uovu huo utafanywa na mtu ambaye amekubalika na watu, msomi ambaye watu wamekiri ujuzi wake, kwa viongozi ambao watu wamekubali uongozi wao, kwa watawala ambao watu wamekubali utawala wao, basi wakati huo nchi itakabiliwa na uharibifu. Hii ni kwa sababu mtu aliyeshika hatamu za uongozi hajatakasika".

1411459

captcha