IQNA

Diplomasia ya Kiislamu

Ayatullah Khamenei: Mashinikizo ya kisiasa yazidishwe dhidi ya Marekani na utawala wa Kizayuni

19:46 - November 06, 2023
Habari ID: 3477851
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza udharura wa kuongezeka mashinikizo ya kisiasa ya Ulimwengu wa Kiislamu dhidi ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ili kusimamisha mauaji yanayofanywa dhidi ya watu wa Gaza na kusema: Iraq, ikiwa nchi muhimu katika eneo la Magharibi mwa Asia, inaweza kuwa na nafasi maalumu katika uwanja huu na kuanzisha mstari mpya katika ulimwengu wa Waarabu na wa Kiislamu.

Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo leo mjini Tehran katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammed Shia Al Sudani na ujumbe anaofuatana nao mjini Tehran. Huku akipongeza misimamo mizuri na dhabiti ya serikali na taifa la Iraq katika kuwaunga mkono watu wa Ukanda wa Gaza, ameashiria hali ya kusikitisha ya eneo hilo na kujeruhiwa kwa mioyo ya watu wote huru kutokana na jinai na ukatili huo na kuongeza kuwa: Tangu siku za mwanzo kabisa za mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel, ushahidi wote ulionyesha ushiriki wa moja kwa moja wa Wamarekani katika usimamizi wa vita hivyo, na wakati vita hivi vikiendelea, vielelezo vya kushriki moja kwa moja Marekani katika kuongoza jinai za utawala wa Kizayuni vinadhihirika na kuonekana zaidi. 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, iwapo hakutakuwapo msaada wa kijeshi na kisiasa kutoka Marekani basi utawala wa Kizayuni wa Israel hautaweza kuendeleza uhalifu wake na kuongeza kuwa: Wamarekani ni washirika halisi wa Wazayuni katika jinai na uhalifu unaofanyika huko Gaza.

Amesisitiza kuwa: Licha ya mauaji yote yanayofanywa huko Gaza, lakini hadi sasa utawala wa Kizayuni wa Israel umeshindwa katika suala hilo kwa sababu haujaweza kurejesha hadhi yake iliyotoweka na hautaweza kufanya hivyo katika siku za usoni.

Ayatullah Ali Khamenei amesisitiza ulazima wa kufanyika juhudi za pande zote za kuzidisha mashinikizo ya kisiasa dhidi ya Marekani na utawala wa Kizayuni ili kukomesha mashambulizi huko Gaza na kusema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Iraq zinaweza kuwa na nafasi na taathira katika uwanja huo.

Ayatullah Khamenei aidha amesema kuhusu ushirikiano wa pande mbili kati ya Iran na Iraq katika nyuga za kiuchumi na kiusalama kwamba: Mapatano yaliyofikiwa baina ya pande mbili yanapaswa kufuatiliwa na kuendelezwa kwa msukumo ule ule wa awali bila ya kupunguza kasi yake.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amewashukuru wananchi na serikali ya Iraq na Waziri Mkuu mwenyewe kwa ukarimu wao, kulinda usalama na kutoa huduma kwa Waislamu waliokwenda Iraq katika kipindi cha Arubaini ya Imam Husseini (as).

/4180241

Habari zinazohusiana
captcha