IQNA

Saudia yatangaza hakuna vizingiti katika idadi ya wanaofanya Ibada ya Umrah

23:01 - August 04, 2021
Habari ID: 3474159
TEHRAN (IQNA)- Wakuu wa Saudi Arabia wametangaza kuwa hakutakuwa na vizingiti katika idadi ya watu wanaotaka kutekeleza Ibada ya Hija ndogo ya Umrah katika mwaka mpya wa Hijria Qamaria unaotazamiwa kuanza Alhamisi ijayo.

Naibu Waziri wa Hija na Umrah Saudia Abdulfattah Mashat amesema hakutakuwa na vingiti katika idadi ya wanaotaka kutekeleza Ibada ya Umrah maadamu washiriki wanatekeleza masharti ya kiafya wakati huu wa janga la COVID-19.

Hivi karibuni pia Wizara ya Hija na Umra ya Saudi Arabia ilitangaza kuwa nchi hiyo itaanza kupokea idadi maalum ya Waislamu wanaokusudia kwenda nchini humo kutekeleza Umrah.

Kwa mujibu wa gazeti la A'kkadh linalochapishwa nchini Saudia, Hisham Saeed, msemaji wa wizara ya Hija na Umra ya nchi hiyo ametangaza kuwa, kuanzia tarehe 10 Agosti idadi ya mahujaji 20,000 kutoka ndani na nje ya nchi wataruhusiwa kutekeleza Hija ndogo ya Umra.

Saeed amesisitiza kuwa, kupitia mpango uliopewa jina la "I'tamarna" mahujaji watazuru miji mitukufu ya Makka na Madina kwa kufuata miiko maalum ya kiafya na kwamba zitafanyika juhudi hatua kwa hatua ili kuongeza idadi ya mahujaji na mazuwari katika awamu zitakazofuatia.

Afisa huyo wa wizara ya Hija na Umra ya Saudi Arabia amebainisha kuwa, nchi ambazo zitaweza kutuma mahujaji kwa ajili ya Umra ni zile ambazo hazijapigwa marufuku na wizara ya afya pamoja na shirika la ndege la Saudia. Hata hivyo hakuashiria ni raia wa nchi gani hasa ambao kwa sasa wataweza kutekeleza ibada hiyo.

Kama ilivyokuwa mwaka jana na kwa uamuzi uliochukuliwa na serikali ya Saudi Arabia, ibada ya Hija ya mwaka huu pia imefanyika kwa kushirikisha mahujaji elfu sitini tu ambao ni raia wa Saudia na wageni waishio nchini humo kwa sasa.

Uendeshaji wa shughuli za Ibada tukufu za Hija na Umra umewekewa masharti na mipaka nchini Saudia katika hali ambayo, hivi karibuni watumiaji wa mitandao ya kijamii katika nchi hiyo wamelalamikia vikali sherehe za misimu na matamasha ya muziki yanayofanyika nchini humo.

3475435

Kishikizo: saudia umrah
captcha