IQNA

Nchi 14 za Afrika zapinga Israel kuwa mtazamaji katika Umoja wa Afrika

22:45 - August 01, 2021
Habari ID: 3474149
TEHRAN (IQNA)- Nchi 14 za Afrika zimetangaza msimamo imara wa kupinga utawala wa haramu wa Israel kuwa mwanachama mtazamaji katika Umoja wa Afrika

Algeria imetangaza kuanzisha rasmi mchakato wa kubuni kundi la Kiafrika litakalofuatilia kutenguliwa uamuzi wa kuruhusiwa utawala haramu wa Israel kuwa mwanachama mtazamaji katika Umoja wa Afrika AU, ili kulinda misingi ya umoja huo inayounga mkono taifa la Palestina.

Nchi 13 nyingine za Umoja wa Afrika yaani, Afrika Kusini, Tunisia, Eritrea, Senegal, Tanzania, Niger, Visiwa vya Comoro, Gabon, Nigeria, Zimbabwe, Liberia, Ushelisheli na Namibia zinapinga vikali suala la utawala wa kibaguzi wa Israel kupewa uanachama wa nchi tazamaji katika umoja huo na bila shaka zitaunga mkono hatua yoyote ya Algeria dhidi ya utawala huo. Namibia imepinga vikali uamuzi huo wa Umoja wa Afrika na kusema unapingana wazi wazi na malengo ya kubuniwa kwake.

Upinzani mkubwa

Msimamo mmoja wa nchi 14 za Umoja wa Afrika dhidi ya Israel kupewa uanachama wa nchi tazamaji katika umoja huo ni dalili ya wazi kwamba kungali kuna upinzani mkubwa dhidi ya utawala wa Kizayuni barani Afrika licha ya juhudi kubwa ambazo zimefanywa na utawala huo kwa ajili ya kujiimarisha barani humo, zikiwmo za kuanzisha uhusiano wa kawaida na nchi kama Sudan na Morocco. Ni kwa miongo mingi sasa ambapo utawala haramu wa Israel umekuwa akifanya juhudi kubwa za kujitoa katika hali ya kutengwa kimataifa kwa kupenya na kujiimarisha barani Afrika na wakati huo huo kutafuta njia za kupora utajiri na maliasili za bara hilo.

Ngome madhubuti

Katika miaka ya mwisho ya utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani, ambaye litoa mchango mkubwa katika kudhamini maslahi ya utawala wa Tel Aviv, rais huyo alishinikiza na hatimaye kuzishawishi nchi za Sudan na Morocco zianzishe uhusiano wa kawaida na utawala huo. Kwa kudhani kuwa sasa uwanja ulikuwa umeandaliwa kwa ajili ya kuimarisha satwa na ushawishi wake barani Afrika, utawala wa Israal ilianzisha juhudi za kutaka kupewa uanachama wa nchi tazamaji katika Umoja wa Afrika. Kinyume na ulivyotarajia, sasa utawala huo unakabiliwa na ngome moja madhubuti kinzani kutoka kwa nchi za Kiafrika ambazo zinapinga vikali uanachama wake katika Umoja wa Afrika na kutaka ufutiliwe mbali mara moja.

Juhudi za kidiplomasia

Akizungumzia karibuni msimamo wa nchi za Afrika, Ramtane Lamamra, Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria amesisitiza kuwa nchi hiyo kamwe haitakaa kimya kuhusiana na hatua ya karibuni ya Umoja wa Afrika ya kuupa utawala huo ghasibu uanachama wa nchi tazamaji bila kushauriana na wanachama wake na kwamba nchi hiyo itaendeleza juhudi za kidiplomasia kwa ajili ya kutenguliwa uamuzi huo.

Utawala wa kibaguzi wa Israel kabla ya hapo ulipewa anwani hiyo ya nchi tazamaji katika Umoja wa Nchi Huru za Afrika OAU lakini ukafutilia mbali mwaka 2002 baada ya kubadilishwa jina la umoja huo kuwa Umoja wa Afrika AU. Huku akisherehekea uanachama huo mpya wa utawala wa Israel katika Umoja wa Afrika, Yair Lapid, Waziri wa Mambo ya Nje wa utawala huo alisema katika taarifa tarehe 22 Julai kuwa siku ya kutangazwa uanachama wa Israel katika Umoja wa Afrika ilikuwa ni siku ya idi na shangwe kwa utawala huo wa kibaguzi. Pamoja na hayo, lakini sasa utawala huo unatarajiwa kupitia siku za jinamizi baada ya nchi 14 wanachama muhimu wa Umoja wa Afrika kupinga uanachama wake na kutaka ufutiliwe mbali mara moja.

Barua ya Hamas

Uanachama wa utawala wa Israel haupingwi tu na nchi za Kiafrika bali nchi na makundi kadhaa ya nje ya bara hilo pia yamepinga uamuzi wa karibuni wa Umoja wa Afrika wa kuupa utawala wa Tel Aviv uanachama wa nchi tazamaji. Ismail Hania, Mkuu wa Ofisi ya Masuala ya Siasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu Hamas, amemwandikia barua ya malalamiko Muossa Faki, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika akilalamikia hatua ya umoja huo ya kuipa Israel uanachama wa nchi tazamaji. Katika barua hiyo, Hania amesema utawala huo ghasibu utatumia vibaya nafasi hiyo kuendeleza mipango yake ya kikoloni, kukalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina na kudumisha jinai zake katika ardhi hizo na dhidi ya taifa la Palestina.

Nchi muhimu

Nukta muhimu hapa ni kwamba, kati ya nchi 14 zinazopinga uanachama wa Israel katika Umoja wa Afrika kuna nchi kadhaa muhimu barani Afrika kama Afrika Kusini ambayo imestawi zaidi kimaendeleo barani humo, Nigeria ambayo ina idadi kubwa zaidi ya watu na Algeria ambayo ni moja ya nchi kubwa zaidi kiardhi barani Afrika. Afrika Kusini imesema, hatua ya karibuni ya Umoja wa Afrika kuhusu utawala wa Israel ni ya kidhalimu na isiyohalalishika. Bila shaka Umoja wa Afrika hautaendelea kupuuza msimamo hasi wa nchi za Kiafrika kuhusiana na uanachama wa Israel katika umoja huo na hatimaye utalazimika tu kubadili uamauzi wake katika uwanja huo.

 

125598

captcha