IQNA

Kenya iko mbioni kuwa kituo cha huduma za kifedha za Kiislamu Afrika

20:07 - August 12, 2020
Habari ID: 3473061
TEHRAN (IQNA) – Kenya inatekeleza mkakati wa kuwa kituo na kitovu cha huduma za kifedha katika eneo zima la Afrika Mashariki na Kati mwa Afrika.

Pamoja na kuwa kwa mujibu wa takwimu rasmi  Waislamu ni takribani asilimia 11 ya watu wote wa Kenya, lakini sekta ya kifedha nchini humo imekuwa mwenyeji wa benki za Kiislamu na huduma za bima za Kiislamu au takaful kwa zaidi ya muongo mmoja.

Hivi sasa taifa hilo la Afrika Mashariki liko mbioni kutekeleza mapendekezo kadhaa ya kisera ili kuimarisha mfumo wa kifedha  za Kiislamu ukiwemo wa huduma za benki, bima ya Kiislamu yaani takaful na soko la hisa la Kiislamu yaani sukuk.

Hatua ya awali ya kuweka sera kwa ajili ya mfumo wa kifedha wa Kiislamu ilianza wakati  suala hilo lilipozingatiwa katika bajeti ya mwaka 2017/18 ambapo Kenya serikali ilitangaza azma ya kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa nchi hiyo inageuka kuwa kitovu cha kieneo cha huduma za Kiislamu za kifedha ili kuvutia wawekezaji wa kigeni.

“Sekta ya fedha ya Kiislamu ni kati ya sekta ambazo serikali ya Kenya inalenga kutumia kuifanya nchi hii iongoze kiuchumi katika eneo,” Luke Ombara, mkurugenzi wa  sera na stratijia katika Mamlaka ya Masoko ya Mitaji (CMA) ameiambia tovuti ya Salaam Gateway. Anasema mkakati kuhusu huduma za kifedha za Kiislamu Kenya ulianza katika muongo wa 90 wakati Benki Kuu ya Kenya ilianza kupokea mapendekezo kutoka kwa wawekezaji. Mwaka 2004, ombi la benki ya kwanza ya Kiislamu, First Community Bank (FCB), lilipokewa. Ombara anasema mfumo wa kifedha wa Kiislamu umejumuishwa katika  ule mpango unaojulikana kama Kenya Vision 2030 ambao ni mpango wa maendeleo ya kiuchumi wa serikali ya Kenya kuendeleza maeneo mbali mbali ya kiuchumi.

Ombara anaongeza kuwa changamoto kubwa katika mfumo wa kifedha wa Kiislamu Kenya ni kuelimisha wananchi wafahamu unavyofanya kazi hasa kwa kuzingatia kuwa ni wa Kiislamu. Halikadhalika anasema Kenya inashirkiana na taasisi za kifedha za Kiislamu za kimataifa ili kuweka viwango kwa mujibu wa vigezo vya kimataifa. Kwa msingi huo Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Benki Kuu ya Kenya ni wanachama wa Bodi ya Huduma za Kifedha za Kiislamu (IFSB) yenye makao yake Malaysia. Hivi sasa kuna benki tatu za Kiislamu Kenya ambazo ni First Community Bank, Gulf African Bank na DIB Bank Kenya ambayo ni tawi la Benki ya Kiislamu ya Dubai. Aidha kuna benki kadhaa za kawaida Kenya ambazo zina matawi ya huduma za kifedha za Kiislamu. Halikadhalika huduma za bima ya Kiislamu Kenya zinatolewa na shirika la Takaful Insurance Afrika. Ombara pia amesema Kenya imeanzisha huduma za Kiislamu katika soko la hisa, mifuko ya malipo ya uzeeni na taasisi za ushirika.

Kenya inalenga kuiwa nchi zilizostawi upya kiviwanda inayotoa huduma za hali ya juu kimaisha kwa raia wake wote ifikapo mwaka 2030 na moja ya hatua zinazochukuliwa ni kufungua milango kwa mfumo wa kifedha wa Kiislamu. “Mfumo wa Kifedha wa Kiislamu utauwezesha uchumi wa Kenya kufikia malengo  ya ustawi. Katika kipindi cha miaka mitatu hadi mitano ijayo, Kenya inalenga kuwa kituo cha kuvutia uwekezaji kutoka nchi za Ghuba ya Uajemi ili waweza kuisaidia kufikia malengo yake ya maendeleo ya mwaka 2030,” amesema Ombara.

3915938

captcha