IQNA

Ujerumani yatafakari kutambua rasmi sikukuu za Kiislamu

11:27 - October 14, 2017
Habari ID: 3471215
TEHRAN (IQNA)-Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere amependekeza kuwa sikukuu za Kiislamu zitambuliwe rasmi na zisherehekewe nchini humo.

Akizungumza siku chache zilizopita katika mkutano wa kampeni katika jimbo la Lower Saxony, De Maiziere, ambaye ni waziri kutoka chama cha Christian Democrat (CDU) cha Kansela Angela Merkel, alisema anakaribisha mazungumzo kuhusu uwezekano wa kutambua rasmi sikukuu za Kiislamu.

"Niko tayari kujadili iwapo tunaweza kutambua siku kuu ya Kiislamu," de Maiziere alisema, na kuongeza kuwa Wakatoliki na Waprotestanti husherehekea sikukuu zao za kidini katika maeneo walikowengi. Ameendelea kwa kuhoji hivi, "Katika maeneo ambayo kuna Waislamu wengi, kwa nini tusiwe na sikukuu za Waislamu?

Kuna Waislamu karibu milioni tano Ujerumani yaani asilimia 5.7 ya watu wote nchini humo na wengi wao ni kizazi cha pili au cha tatu cha Waturuki waliohamia nchini humo katika muongo wa 60.

Kufuatia pendekezo hilo, Aiman Mazyek, mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Ujerumani amesema hatua kama hiyo itapelekea Waislamu nao wajihisi wanakubalika katika jamii ya Wajerumani.

Amesema iwapo sikukuu za Kiislamu zitatambuliwa kama siku za mapumziko ya umma katika majimbo yenye Waislamu wengu Ujerumani, jambo hilo litaondoa changamoto nyingi ambazo Waislamu hukumbana nazo wakati wa sherehe zao za kidini. Amesema Waislamu hulazimika kuenda kazini au shuleni wakati wa sikukuu za Kiislamu katika hali ambayo wakati wa sikukuu za Kikristo huwa likizo za kitaifa.

Hatahivyo, pendekezo la de Maiziere halikupata uungaji mkono mkubwa katika chama chake cha CDU. Bernd Althusmann anayegombea kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi wa baraza la jimbo la Lower Saxony amekosoa vikali pendekezo hilo na kusema hakuna haja ya kubadilisha mfumo ulioko hivi sasa wa sikukuu nchini Ujerumani.

3464154

captcha