IQNA

Nchi za Kiislamu Zataka Mauaji ya Waislamu Myanmar yasitishwe mara moja

11:47 - September 11, 2017
Habari ID: 3471167
TEHRAN (IQNA)-Viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC wamesisitiza kuhusu umuhimu wa kuchukuliwa hatua za haraka kumaliza mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar.

Wakuu wa nchi za Kiislamu wametoa tamko hilo Jumapili pembizoni mwa mkutano wa kwanza wa viongozi wa nchi wanachama wa OIC kuhusu sayansi na teknolojia katika mji mkuu wa Kazakhstan, Astana.

Taarifa hiyo imetaka kuwepo ushirikiano zaidi miongoni mwa nchi za Kiislamu katika kutuma misaada ya kibinadamu kuwasaidia Waislamu wa jamii ya Rohingya wanaodhulumiwa. Viongozi hao wa nchi za OIC wamebainisha pia wasiwasi wao kuhusu jinai zinazoendelea dhidi ya Waislamu Warohingya.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu aidha imeafiki mpango huo ambao umewasilishwa na Umoja wa Mataifa pamoja na taasisi kadhaa za kimataifa ambao unajumuisha kupelekea misaada ya dharura kwa wakimbizi laki tatu wa jamii ya Waislamu wa kabila la Rohingya walikimbilia hifadhi nchini Bangladesh kufuatia kuangamizwa kwa umati wenzao nchini Myanmar. Kati ya misaada hiyo ni vyakula, maji na dawa.

Akihutubia kikao hicho, Rais Hassan Rouhani wa Iran amesisitizia ulazima wa umoja na ushirikiano wa nchi za Waislamu ili kuondoa machafuko duniani na kupatikane amani ya kudumu.

Rais Rouhani amesema, udhaifu, kubaki nyuma na kukosekana umoja wa nchi za Waislamu ni mambo ambayo yanapelekea iwe vigumu kufikia amani na ustawi jumuishi. Rais wa Iran amesema, ushirikiano wa nchi za Ulimwengu wa Kiislamu ni jambo linaloweza kupelekea kuangamizwa ujinga, umasikiini na vita duniani.

Aidha amesema nchi za Kiislamu leo zinahitaji umoja kwani zinakabiliana na migogoro kadhaa kama vile jinai za Israel dhidi ya Wapalestina, ukatili wa Mabuddha wenye misimamo mikali dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya pamoja na maafa ya kibinadamu yaliyosababishwa na makundi yenye misimamo mikali huko Syria na Iraq na vile vile kuendelea hujuma za Saudia nchini Yemen.

Tume ya Wakimbizi ya Umoja wa Maaifa UNHCR inasema katika kipindi cha wiki mbili zilizopita karibu Waislamu laki tatu wameingia Bangladesh wakikimbia mauaji ya kimbari Myanmar.

Taarifa zinasema tokea Agosti 25 wakati Jeshi la Myanmar lilipoanzisha hujuma dhidi ya Waislamu katika jimbo la Rakhine, Waislamu zaidi ya elfu sita wameuawa kwa umati na wengine elfu nane wamejeruhiwa.

Katika miaka ya karibuni, Waislamu wengi wa kabila la Rohingya nchini Myamnar wameuawa au kulazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za jirani kutokana na mashambulio ya Mabuddha wenye misimamo ya kufurutu mpaka wanaoungwa mkono na serikali ya nchi hiyo.

3640403


captcha